Watu sita akiwemo Kassim Kongwa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka ya kuiba lita 2,800 za mafuta ya ghafi yenye thamani ya Sh milioni 26, yanayodaiwa kuwa mali ya Kampuni ya Mikoani Edible Oil and Detergents Limited.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni kibarua wa Kampuni ya Azania, Hemed Abdallah, Hassan Kimoge, Juma Issah, Halfan Halfan maarufu kama Ruba, Maria Gulaba ambaye ni opereta wa kiwanda hicho, pamoja na mlinzi Jafar Molel.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana jioni na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Anna Magutu, ambapo upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili Kasala alidai kuwa kati ya Juni 2 na 4, 2026, jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa nia ovu na kuhusika katika wizi wa mafuta ya ghafi ya kampuni hiyo.
Ilidaiwa kuwa Juni 4, 2026, katika eneo la Mtaa wa Moringe, Wilaya ya Temeke, walitekeleza wizi wa lita 2,800 za mafuta ya ghafi zenye thamani ya Sh milioni 26.
Mbali na shtaka la wizi, washtakiwa hao pia wanakabiliwa na shtaka la utakatishaji fedha. Upande wa mashtaka ulidai kuwa walijipatia mafuta hayo huku wakijua yalitokana na kosa tangulizi la wizi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi zinazojumuisha shtaka la utakatishaji fedha.
Upande wa Jamhuri ulieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo kesi imeahirishwa hadi Juni 30, 2026, itakapotajwa tena mahakamani.
Washtakiwa wote wamepelekwa mahabusu kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.




